ASANTENI SANA NA MUNGU AWABARIKI ZAIDI NA ZAIDI
Naomba kuchukua fursa hii kuwashukuru wapendwa wote mlionitakia heri katika siku yangu ya kuzaliwa. Mungu awabariki zaidi na zaidi. Hata kama hatuonani kila siku lakini hilo halipotezi ukweli kwamba sisi ni marafiki wa kweli na tutabaki hivyo.
Tafakuri yangu katika siku ya kuzaliwa: Huyu anayeitwa Yesu Kristo, katika utumishi wake hapa duniani zaidi ya miaka 2000 iliyopita, alitumia miaka 3 kufanya yote aliyoyafanya na kutuachia legacy (urithi) ambao ni uhalisia na unaishi hata leo na utaendelea kubaki hivyo kwa vizazi vijavyo.
Baada ya pekua pekua, nilishafahamu na nikatumia muda kutafakari ufahamu huu, kwamba kwa yote aliyoyatenda Yesu Kristo akiwa hapa duniani aliyatenda akiwa kijana, tena kijana kwa mujibu wa Sera ya Vijana ya Mwaka 2007. Yesu Kristo alianza kufanya kazi yake akiwa na miaka 30 na aliitenda kwa miaka takribani 3 na kuhitimisha kazi yake akiwa na miaka 33.
Hoja yangu hapa si kujadili juu ya Yesu ni nani na utumishi wake duniani, hoja yangu ni tafakuri kwetu vijana, Je mpaka sasa tumejiwekea malengo ya kutimiza? Je tungesema tufunge hesabu zako leo unadhani ungekuwa umetusaidiaje wanadamu? Hivi ungekuwa umetuachia nini cha kukukumbuka? Tuache wanadamu wa dunia nzima, tuseme, basi watanzania, au watanzania ni wengi tuseme mtaani kwako, na mitaa nayo ni mikubwa, tuseme kazini, kijiweni, shuleni kwako, kwa rafiki, ndugu na jamaa zako.
Je tunaishi kwa malengo, je tunayaishi malengo yetu? Je tuna ndoto? Ulitaka kuwa rubani, je unaelekea huko? Ulitaka kuwa mwanamuziki, je unapiga hata ala mbili tatu kwa uhodari? Je unaelekea elekea huko? Ulitaka kuwa mtu mwenye mchango kwa shule, jamii au Taifa lako, mchango wa aina yoyote ile, Je umeanza kutoa mchango wako.
Simamia ndoto zako, ishi malengo yako na enenda katika namna ambayo itakufikisha katika tarajio lako tarajiwa kama mtu mwenye mchango kwa jamii yako. Kumbuka tunakua pamoja, Rai yangu kwetu sote, kwa uhalali na dhamira safi tujitahidi kuwezeshana ili tukue pamoja, tufanikiwe pamoja, asipatikane mmoja kuwa mzigo miongoni mwetu, kila mmoja wetu awe fursa, awe ngazi, awe kivuko, awe mlango, awe ufunguo wa mafanikio ya mwingine. Huo ndio utu wa kweli.
Ndoto zetu zitakuwa uhalisia tukiwa na Katiba Mpya na Bora ambayo inayokana na Maoni yetu na sisi tukiwa waandishi wakuu maana huo ndio mustakabali wetu. Isome Katiba Inayopendekezwa na uilinganishe na Rasimu ya Warioba, kisha ukishajiridhisha tujadiliane kwa hoja na sababu.
Mwisho ukimaliza kusoma tafakuri yangu ya Siku ya Kuzaliwa, Jiulize je Umeshajiandikisha kupiga kura kwa uchaguzi wa Serikali za Mitaa? Kama bado tafadhali nenda upesi, kama tayari pita tena ukathibitishe kama jina lako liko. Pia usisahau kufuatilia huyu "escrow" na uwe na uwezo wa kufuatilia hoja kadhaa kwa wakati mmoja bila ya kuondolewa kwenye reli ya hoja za msingi. Tanzania itajengwa na wenye Moyo na Imani.
Sambaza Uzalendo, huu ndio upendo kwa Taifa letu.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
No comments :
Post a Comment