KUIMARISHA MAMLAKA YA WANANCHI NI PAMOJA NA HAKI YA KUMWAJIBISHA MBUNGE: HUU NI UHALISIA NA SI NADHARIA

No comments

Katiba ya kimageuzi inaweka uhusiano wa moja kwa moja kati ya wanaochaguliwa na wanaochagua
Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya Mwaka 1977 Toleo la 2005, inaeleza bayana kwamba wananchi ndio msingi wa Mamlaka yote, na ieleweke kwamba tunapozungumzia Mamlaka yote tunamaanisha Serikali, Bunge na Mahakama. Katiba ya 1977 inaendelea kusema Serikali na vyombo vyake vyote vitapata Mamlaka yake kutoka kwa wananchi na kwamba lengo kuu la Serikali ni ustawi wa wananchi na wananchi watashiriki katika shughuli za serikali kwa mujibu wa masharti ya Katiba hii.
Lakini karibu wote watakubaliana nami kwamba misingi hii muhimu iliyowekwa na Katiba yetu ya Mwaka 1977 na ambayo inatumika sasa, kwa kiasi fulani ilikuwa inaminywa na masharti vikwazo ambavyo viko hata leo. Mfano mzuri wa vikwazo ni pamoja na Ibara ya 21 inayosema “bila ya kuathiri masharti ya ibara ya 39, ya 47 na 67 ya Katiba hii na ya sheria za Nchi kuhusiana na masharti ya kuchagua na kuchaguliwa, au kuteua na kuteuliwa kushiriki katika shughuli za utawala wa Nchi, kila raia wa Jamhuri ya Muungano anayo haki ya kushiriki katika shughuli za utawala wa Nchi, ama moja kwa moja au kwa kupitia wawakilishi waliochaguliwa na wananchi kwa hiyari yao, kwa kuzingatia utaratibu uliwekwa na sheria au kwa mujibu wa sheria”.
Huwezi kuwa na haki inayotolewa kwa raia halafu ukaipoka kwa kuiwekea masharti mengine ambayo yanaminya haki ya kushiriki moja kwa moja. Ukizingatia pia uandishi mzuri wa masharti ya haki za binadamu, ni vema na ndio mtindo wa kiuandishi wa kileo kwamba haki inatolewa moja kwa moja na si kwa mtindo wa kiuandishi ambao Katiba ya sasa inautumia hasa kwenye Ibara ya 21.
Tofauti na Katiba Inayotumika sasa ya Mwaka 1977, Rasimu ya Katiba Mpya Toleo la Pili imerejesha haki hii kwa raia moja kwa moja bila masharti yanayokwaza au kwa kiingereza huitwa “clawback clauses”.
Najaribu kuonesha Mamlaka ya wananchi na uhusiano unaopaswa kuwepo kati ya Mamlaka ya Nchi na vyombo vyake vyote na wananchi ambao kwa ujumla wao wanatoa dhamana kwa watumishi na viongozi wa mihimili yote ya dola. Ni kwa msingi huu ninajenga hoja kwamba kama wananchi kweli kweli ndio msingi wa Mamlaka yote, mamlaka haya hayako kinadharia bali yako kiuhalisia kwa hakika. Kama ambavyo ni uhalisia kwamba Serikali kwa maana ya Rais na Bunge pamoja na wabunge hupata madaraka hayo kutoka kwa wananchi, sidhani kama itakuwa ni nadharia kwa wananchi kuwawajibisha watumishi na viongozi kwa utaratibu wa Kikatiba na kisheria.
Haki ya Kumwajibisha Mbunge
Haki ya kumwajibisha Mbunge ni haki ya wananchi kumuondoa mbunge kutoka kwenye nafasi yake baada ya kupoteza imani naye. Haki hii huwa ni ya moja kwa moja kwa wananchi kumpigia kura ya maoni ya kutokuwa na imani naye, baada ya kura hii na nafasi kuwa wazi, kulingana na mazingira ya nchi husika mambo kadhaa hutokea, ama huitishwa uchaguzi mdogo kujaza nafasi iliyoachwa au katika mfumo ambao wananchi huchagua vyama basi chama kitatoa jina la mwakilishi mpya au mgombea aliyefuatia kwa kura wakati wa uchaguzi uliopita atajaza nafasi hiyo. Katika utaratibu wa kujaza nafasi kuna uzoefu mbalimbali na huwa ni vema taratibu hizi zikawekwa kwenye Sheria za nchi na kulingana na mazingira na wakati zikabadilishwa kama itakavyoonekana inastahili.
Msingi wa dhana hii ni kwamba mchaguliwa kwa mfano mbunge, anaendelea kuwajibika kwa waliompa dhamana wakati wote na akienda kinyume na matakwa yao basi wanaweza kumuondoa.
Rasimu ya Katiba Mpya Toleo la Pili ile maarufu kama Rasimu ya Warioba iliweka masharti ya wananchi kumwajibisha Mbunge wao. Kama mbunge atakwenda kinyume na matakwa ya wananchi katika jimbo husika, baada ya utaratibu wa kisheria kufuatwa basi mbunge huyo ataondolewa. Maoni haya waliyatoa wananchi ambao kwa sauti moja walionesha kukerwa na vitendo vya wabunge wao kutokuwa wawakilishi wazuri, ama kutokuonekana jimboni kwa kipindi kirefu ama kutokuonekana bungeni lakini pia kuzungumza hoja ambazo hazina maslahi kwa jimbo na Taifa kwa ujumla.
Nchi zenye Masharti ya Wananchi kumuondoa Mbunge
Haki ya kumwajibisha mbunge sio jambo geni na hata majirani zetu Kenya wana masharti haya kwenye Katiba yao, Ibara ya 105 ya Katiba ya Kenya inaweka bayana haki ya kumwajibisha Mbunge. Kule Ethiopia pia jambo hili liko Kikatiba, ukisoma Katiba ya Ethiopia katika Ibara yake ya 12(2) inasomeka wananchi wanaweza kumuondoa mwakilishi wao wakati wowote wanapo poteza imani naye. Katika majimbo kule India wananchi wanaweza kumwajibisha Mbunge wao. Kule Uswizi kati ya majimbo yote yanayounda Shirikisho la Uswizi majimbo sita yanayo haki ya kumwajibisha mbunge.
Kule Marekani katika majimbo 18 kuna haki ya kumwajibisha mbunge. Na imekuwa ikitumika haki hii kuwaondoa wawakilishi ambao wanakwenda kinyume na matakwa ya wananchi. Katika majimbo hayo 18 haki hii inakwenda mpaka katika ngazi ya Mkuu wa Jimbo au kwa kiingereza Governor pamoja na wajumbe wa vyombo vya uwakilishi na kutunga sheria. Ningependa kusisitiza hapa, kule Marekani haki ya kuwawajibisha waliopewa dhamana haishii tu kwa wachaguliwa, bali inaendelea pia kwa watendaji wa mihimili mingine ikiwemo Serikali na Mahakama. Mfano wa Majimbo ambayo wananchi wanaweza kuwafukuza kazi watendaji wowote wale katika mihimili yote mitatu ya majimbo ni pamoja na Alizona, California, Colorado, Georgia, Montana, New Jersey, Nevada, North Dacota, Oregon na Wisconsin. Haya sio maigizo au nadharia ni uhalisia kabisa.
Kule katika Nchi ya Peru, pia masharti haya yanafanya kazi na kinachohitajika ni uwepo wa kusudio la kumuondoa mbunge ambalo sharti litimize kigezo cha kukusanya saini za zaidi ya asilimia 50 ya wapiga kura walioshiriki katika uchaguzi uliopita.
Mwaka 2004 kule Venezuela kulitaka kutokea tukio la kihistoria ambapo kulikuwa na kusudio la kumuondoa Rais wa Venezuela na wananchi wapatao milioni mbili na nusu waliweka saini zao kuanzisha mchakato wa kumuondoa Rais wao, mpaka mwisho zoezi halikuwezekana lakini tayari waliotaka Rais aondoke walishafika asilimia 40.6 chini ya kiwango kilichohitajika cha asilimia 50.
Ziko aina mbili za kuwawajibisha wabunge, moja ni kumuondoa mwakilishi katika ngazi yoyote na wananchi wakishiriki kuanzia katika ngazi ya kusudio la kumuondoa mpaka katika ngazi ya kufanya uamuzi wa kumuondoa ambayo huhitimishwa na kura ya maoni. Aina ya pili, ni pale ambapo, wananchi wanashiriki katika mojawapo ya ngazi ama ya kusudio au wakati wa kufanya maamuzi.
Nchi nyingine zaidi ukiacha ambazo nimeshazitaja ambazo Katiba zao zina masharti ya kuwawajibisha kwa maana ya kuwaondoa wawakilishi au wabunge wao ni pamoja na Equador, Cuba, Belarus, Kiribati, Nigeria, Palau, Argentina, Colombia, Austria, Ujerumani, Iceland, Romania, Serbia, Uganda na Taiwan.
Katiba Inayopendekezwa Imefutilia mbali masharti haya ya wananchi kuwawajibisha wabunge, tendo hili ni kinyume na maoni ya wananchi na kinalenga kutweza mamlaka ya wananchi na kinapaswa kujadiliwa kwa hoja na kupingwa kwa hoja na sababu na tutakapofika kwenye kura ya maoni tunapaswa kufanya uamuzi sahihi ili tusipate Katiba ya watawala bali Katiba ya wananchi na inayolinda maslahi mapana ya wananchi na inayoweka misingi ya kuwawajibisha viongozi na watumishi wa umma.
UKIMALIZA KUSOMA SAMBAZA UJUMBE HUU KWA WENZAKO WENGI ZAIDI

No comments :

Post a Comment