Monday, December 15, 2014

Natanguliza shukrani

TUNAHITAJI KUWAFIKIA WATU WENGI ZAIDI "LIKE" YAKO KWA UKURASA WANGU ITAPELEKA MAARIFA KWA WANANCHI WENGI ZAIDI. BAADA YA KU-LIKE *SHARE*

Tunaendelea vema, nafarijika na wote mnaounga mkono kwamba kuna umuhimu wa wananchi kueleweshana, kujadiliana, kufundishana na kutafakari kwa pamoja juu ya Mchakato wa kupata Katiba Mpya. 

Ili tuwafikie watanzania wengi zaidi ndani na nje ya nchi naomba tupateLIKES nyingi zaidi kwa page hii

---->>> Humphrey Polepole <<<----

ili kuwafikia na kuwasambazia uzalendo ambao ndio upendo kwa Taifa letu. Mpaka sasa tumeweza kuwafikia watu elfu 25,000 (page coverage). Naomba tusaidiane kupata LIKES 4000 zaidi wiki hii ili tufike LIKES 10,000 na hivyo kuwafikia watu wengi zaidi na maarifa ya elimu ya uraia juu ya mchakato wa kupata Katiba Mpya.

Nikusihi pia, Usikose kesho Alhamis kupata Nakala yako ya Gazeti la RAI huko ufafanuzi unaendelea.

Natanguliza shukrani

Kwa wale wanathamini kazi niitendayo naomba SHARE ujumbe huu

Kwa wale wanathamini kazi niitendayo naomba SHARE ujumbe huu
Kama sehemu ya ushiriki na mchango wangu katika Mchakato wa Katiba Mpya ni kuuelimisha umma wa watanzania juu ya mchakato wa kupata Katiba Mpya kwa kuandika Makala Maalum za kiuchambuzi kuhusu mchakato na maudhui ya mchakato.
Kila wiki ninaandikia Gazeti ya RAI kila Alhamis na Gazeti la Mwananchi kila Jumapili.
Kazi ninayoifanya ni ya kujitolea na ni kwa mapenzi yangu mema na kama mchango wangu mdogo ili sisi sote kama Taifa tufikie lengo letu la pamoja la kupata Katiba Mpya. Kazi hii sio rahisi hata kidogo, ni ngumu na ninaifanya kiubishi ubishi nikiamini watanzania wenzangu wana haki ya kujua taarifa za mchakato kutoka pande zote za shilingi.
Kwa kazi hii sihitaji malipo ya aina yoyote isipokuwa moja tu, kwamba haijalishi msimamo wowote ulio nao katika mchakato lakini nitendee haki kwa kusoma maudhui ya mchakato wa Katiba Mpya, ambayo ni pamoja na Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, Sheria ya Kura ya Maoni, Katiba ya 1977, Rasimu ya Katiba Toleo la Pili, Katiba Inayopendekezwa na ukipata muda nitashukuru na nitapata faraja kama ukisoma maandiko niandikayo.
Naomba ieleweke, simlazimishi mtu kusoma niandikacho bali kwa heshima kubwa ninawakaribisha kusoma maandiko yangu, napenda kukosolewa kwa hoja, kwa sababu, napenda tujadiliane, napenda sote tuujue ukweli. Imani yangu ni kwamba sote tukishiriki, tukijadiliana, tukiulizana maswali yasiyo mepesi na tukipeana majibu yasiyo mepesi.
Kwa wale mnaothamini mchango wangu mdogo naomba Muusambaze Ujumbe huu kwa ku-SHARE na watu wengi zaidi pamoja na Makala yangu ya Gazeti la Mwananchi Jumapili iliyopita ambayo nimeiambatisha hapa.

KUIMARISHA MAMLAKA YA WANANCHI NI PAMOJA NA HAKI YA KUMWAJIBISHA MBUNGE: HUU NI UHALISIA NA SI NADHARIA


Katiba ya kimageuzi inaweka uhusiano wa moja kwa moja kati ya wanaochaguliwa na wanaochagua
Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya Mwaka 1977 Toleo la 2005, inaeleza bayana kwamba wananchi ndio msingi wa Mamlaka yote, na ieleweke kwamba tunapozungumzia Mamlaka yote tunamaanisha Serikali, Bunge na Mahakama. Katiba ya 1977 inaendelea kusema Serikali na vyombo vyake vyote vitapata Mamlaka yake kutoka kwa wananchi na kwamba lengo kuu la Serikali ni ustawi wa wananchi na wananchi watashiriki katika shughuli za serikali kwa mujibu wa masharti ya Katiba hii.
Lakini karibu wote watakubaliana nami kwamba misingi hii muhimu iliyowekwa na Katiba yetu ya Mwaka 1977 na ambayo inatumika sasa, kwa kiasi fulani ilikuwa inaminywa na masharti vikwazo ambavyo viko hata leo. Mfano mzuri wa vikwazo ni pamoja na Ibara ya 21 inayosema “bila ya kuathiri masharti ya ibara ya 39, ya 47 na 67 ya Katiba hii na ya sheria za Nchi kuhusiana na masharti ya kuchagua na kuchaguliwa, au kuteua na kuteuliwa kushiriki katika shughuli za utawala wa Nchi, kila raia wa Jamhuri ya Muungano anayo haki ya kushiriki katika shughuli za utawala wa Nchi, ama moja kwa moja au kwa kupitia wawakilishi waliochaguliwa na wananchi kwa hiyari yao, kwa kuzingatia utaratibu uliwekwa na sheria au kwa mujibu wa sheria”.
Huwezi kuwa na haki inayotolewa kwa raia halafu ukaipoka kwa kuiwekea masharti mengine ambayo yanaminya haki ya kushiriki moja kwa moja. Ukizingatia pia uandishi mzuri wa masharti ya haki za binadamu, ni vema na ndio mtindo wa kiuandishi wa kileo kwamba haki inatolewa moja kwa moja na si kwa mtindo wa kiuandishi ambao Katiba ya sasa inautumia hasa kwenye Ibara ya 21.
Tofauti na Katiba Inayotumika sasa ya Mwaka 1977, Rasimu ya Katiba Mpya Toleo la Pili imerejesha haki hii kwa raia moja kwa moja bila masharti yanayokwaza au kwa kiingereza huitwa “clawback clauses”.
Najaribu kuonesha Mamlaka ya wananchi na uhusiano unaopaswa kuwepo kati ya Mamlaka ya Nchi na vyombo vyake vyote na wananchi ambao kwa ujumla wao wanatoa dhamana kwa watumishi na viongozi wa mihimili yote ya dola. Ni kwa msingi huu ninajenga hoja kwamba kama wananchi kweli kweli ndio msingi wa Mamlaka yote, mamlaka haya hayako kinadharia bali yako kiuhalisia kwa hakika. Kama ambavyo ni uhalisia kwamba Serikali kwa maana ya Rais na Bunge pamoja na wabunge hupata madaraka hayo kutoka kwa wananchi, sidhani kama itakuwa ni nadharia kwa wananchi kuwawajibisha watumishi na viongozi kwa utaratibu wa Kikatiba na kisheria.
Haki ya Kumwajibisha Mbunge
Haki ya kumwajibisha Mbunge ni haki ya wananchi kumuondoa mbunge kutoka kwenye nafasi yake baada ya kupoteza imani naye. Haki hii huwa ni ya moja kwa moja kwa wananchi kumpigia kura ya maoni ya kutokuwa na imani naye, baada ya kura hii na nafasi kuwa wazi, kulingana na mazingira ya nchi husika mambo kadhaa hutokea, ama huitishwa uchaguzi mdogo kujaza nafasi iliyoachwa au katika mfumo ambao wananchi huchagua vyama basi chama kitatoa jina la mwakilishi mpya au mgombea aliyefuatia kwa kura wakati wa uchaguzi uliopita atajaza nafasi hiyo. Katika utaratibu wa kujaza nafasi kuna uzoefu mbalimbali na huwa ni vema taratibu hizi zikawekwa kwenye Sheria za nchi na kulingana na mazingira na wakati zikabadilishwa kama itakavyoonekana inastahili.
Msingi wa dhana hii ni kwamba mchaguliwa kwa mfano mbunge, anaendelea kuwajibika kwa waliompa dhamana wakati wote na akienda kinyume na matakwa yao basi wanaweza kumuondoa.
Rasimu ya Katiba Mpya Toleo la Pili ile maarufu kama Rasimu ya Warioba iliweka masharti ya wananchi kumwajibisha Mbunge wao. Kama mbunge atakwenda kinyume na matakwa ya wananchi katika jimbo husika, baada ya utaratibu wa kisheria kufuatwa basi mbunge huyo ataondolewa. Maoni haya waliyatoa wananchi ambao kwa sauti moja walionesha kukerwa na vitendo vya wabunge wao kutokuwa wawakilishi wazuri, ama kutokuonekana jimboni kwa kipindi kirefu ama kutokuonekana bungeni lakini pia kuzungumza hoja ambazo hazina maslahi kwa jimbo na Taifa kwa ujumla.
Nchi zenye Masharti ya Wananchi kumuondoa Mbunge
Haki ya kumwajibisha mbunge sio jambo geni na hata majirani zetu Kenya wana masharti haya kwenye Katiba yao, Ibara ya 105 ya Katiba ya Kenya inaweka bayana haki ya kumwajibisha Mbunge. Kule Ethiopia pia jambo hili liko Kikatiba, ukisoma Katiba ya Ethiopia katika Ibara yake ya 12(2) inasomeka wananchi wanaweza kumuondoa mwakilishi wao wakati wowote wanapo poteza imani naye. Katika majimbo kule India wananchi wanaweza kumwajibisha Mbunge wao. Kule Uswizi kati ya majimbo yote yanayounda Shirikisho la Uswizi majimbo sita yanayo haki ya kumwajibisha mbunge.
Kule Marekani katika majimbo 18 kuna haki ya kumwajibisha mbunge. Na imekuwa ikitumika haki hii kuwaondoa wawakilishi ambao wanakwenda kinyume na matakwa ya wananchi. Katika majimbo hayo 18 haki hii inakwenda mpaka katika ngazi ya Mkuu wa Jimbo au kwa kiingereza Governor pamoja na wajumbe wa vyombo vya uwakilishi na kutunga sheria. Ningependa kusisitiza hapa, kule Marekani haki ya kuwawajibisha waliopewa dhamana haishii tu kwa wachaguliwa, bali inaendelea pia kwa watendaji wa mihimili mingine ikiwemo Serikali na Mahakama. Mfano wa Majimbo ambayo wananchi wanaweza kuwafukuza kazi watendaji wowote wale katika mihimili yote mitatu ya majimbo ni pamoja na Alizona, California, Colorado, Georgia, Montana, New Jersey, Nevada, North Dacota, Oregon na Wisconsin. Haya sio maigizo au nadharia ni uhalisia kabisa.
Kule katika Nchi ya Peru, pia masharti haya yanafanya kazi na kinachohitajika ni uwepo wa kusudio la kumuondoa mbunge ambalo sharti litimize kigezo cha kukusanya saini za zaidi ya asilimia 50 ya wapiga kura walioshiriki katika uchaguzi uliopita.
Mwaka 2004 kule Venezuela kulitaka kutokea tukio la kihistoria ambapo kulikuwa na kusudio la kumuondoa Rais wa Venezuela na wananchi wapatao milioni mbili na nusu waliweka saini zao kuanzisha mchakato wa kumuondoa Rais wao, mpaka mwisho zoezi halikuwezekana lakini tayari waliotaka Rais aondoke walishafika asilimia 40.6 chini ya kiwango kilichohitajika cha asilimia 50.
Ziko aina mbili za kuwawajibisha wabunge, moja ni kumuondoa mwakilishi katika ngazi yoyote na wananchi wakishiriki kuanzia katika ngazi ya kusudio la kumuondoa mpaka katika ngazi ya kufanya uamuzi wa kumuondoa ambayo huhitimishwa na kura ya maoni. Aina ya pili, ni pale ambapo, wananchi wanashiriki katika mojawapo ya ngazi ama ya kusudio au wakati wa kufanya maamuzi.
Nchi nyingine zaidi ukiacha ambazo nimeshazitaja ambazo Katiba zao zina masharti ya kuwawajibisha kwa maana ya kuwaondoa wawakilishi au wabunge wao ni pamoja na Equador, Cuba, Belarus, Kiribati, Nigeria, Palau, Argentina, Colombia, Austria, Ujerumani, Iceland, Romania, Serbia, Uganda na Taiwan.
Katiba Inayopendekezwa Imefutilia mbali masharti haya ya wananchi kuwawajibisha wabunge, tendo hili ni kinyume na maoni ya wananchi na kinalenga kutweza mamlaka ya wananchi na kinapaswa kujadiliwa kwa hoja na kupingwa kwa hoja na sababu na tutakapofika kwenye kura ya maoni tunapaswa kufanya uamuzi sahihi ili tusipate Katiba ya watawala bali Katiba ya wananchi na inayolinda maslahi mapana ya wananchi na inayoweka misingi ya kuwawajibisha viongozi na watumishi wa umma.
UKIMALIZA KUSOMA SAMBAZA UJUMBE HUU KWA WENZAKO WENGI ZAIDI

KAMA TUTAUISHI MUUNGANO TUNA BUDI KUSEMA KWELI KUULINDA


KAMA TUTAUISHI MUUNGANO TUNA BUDI KUSEMA KWELI KUULINDA

Katiba Inayopendekezwa inadhoofisha Muungano


Katiba inayopendekezwa kwa mujibu wa maelekezo na matakwa ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba Sura ya 83 imekwisha kabidhiwa kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano Mh. Dkt. Jakaya Kikwete pamoja na Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) Dkt. Ali Mohamed Shein. Sote tu mashuhuda, wale waliokuwa uwanja wa Jamhuri pale Mji Mkuu Dodoma na wale tuliokuwa mbele ya runinga zetu, tukifuatilia hatua kwa hatua katika ratiba ya Makabidhiano hayo. Ni kwa hakika tuna Katiba Inayopendekezwa, nadhani nikianza hivi sitaonekana mbishi, kweli mimi sio mbishi, ninafuata sheria, ninatii mamlaka ya nchi na ninawaheshimu viongozi wangu.

Baada ya kusema hayo nikiri kwamba, ninaipenda nchi yetu Tanzania, sijaota ndoto ya nchi nyingine bora kuliko Tanzania, nimezunguka dunia yote, kote kuzuri na kule kwenye changamoto bado nikiwa kote huko natamani siku ziende nirudi kwetu nyumbani. Ninasema haya kumaanisha niyafanyayo, sisukumwi na mihemko ya wakati, sisukumwi na itikadi za vyama vya siasa tena ambavyo kwa kiasi kikubwa ambavyo vinaendelea kutukwaza watanzania kwa kuweka mbele maslahi yao na kuacha nyuma maslahi ya Taifa. Hata kwenye chama ambacho mimi ni mwanachama wanajua sikubaliani na maelekezo yanayokwenda kinyume na maslahi ya wananchi. Nifanyacho hakipati maelekezo ya taasisi yoyote, wala mtu yeyote bali sauti za watanzania ambao naendelea kuwakumbuka wakitoa maoni yao. Siamini kwamba tulikwenda kuwahadaa ili tuhalalishe letu, unajua ugumu ninaoupata hausimuliki, napitia kipindi kigumu na kinachoambatana na msongo mkubwa wa mawazo.

Kwa kawaida mimi huwa si mtu wa mawazo, nastahimili majaribu ya wakati lakini kipindi hiki najihoji, ilikuwaje nikapata bahati mbaya hii? Hili nitaendelea kulisema moyoni mwangu na kwa watu wangu wa karibu, “aliposema nenda ukajifunze” na akarudia mara kadhaa tena “unajifunza lakini?” nikajibu kwa woga nikitoa uhakika kwamba ninafanya kila lililo ndani ya uwezo wangu wa kibinadamu kuelewa mambo, kuuliza, kusoma, kuongea na kila ambaye anaweza kuwa chanzo na msingi wa taarifa sahihi, taarifa ziletazo maarifa ya kweli. Ningesema nizungumze kwa kiingereza kuonesha msisitizo ningesema “I did all that”.

Nilikuwa katika kila majadiliano katika Tume ya Katiba, na sio vibaya nikisema nilikuwa Katibu wa Kamati ya Muungano, nilijua taarifa zote za wazi na za siri, nakumbuka maoni yote ya viongozi walioko madarakani na waliostaafu, nakumbuka sana. Nilikuwa Katibu wa Kamati ya Wenyeviti wa Kamati zote za Tume ya Katiba, nakumbuka kazi kubwa walifanya, nakumbuka vikao vyao virefu, vilivyokuwa vimejaa uzalendo mkubwa wa kutoa mapendekezo ya kutupatia Tanzania Mpya sasa na kwa miaka 50 ijayo. Nayasema haya nikiwa mtu mwenye kifua, nayasema kwa jumla jumla tu ili kujaribu kuonesha nikisemacho sijaokota kwenye mkutano wa hadhara, au kongamano la Azaki au kutoka kwa mtu fulani au taasisi fulani na kwa maslahi fulani. Nikisemacho ni kweli, na ni kweli tupu, sikufanya mzaha nilipokula kiapo, niliapa kweli mbele ya Mkuu wa Nchi na Mbele ya Mungu wangu ninayemuamini, na ukijumlisha na kuaswa na kila mtu wa kila rika, wakiwemo wazazi wangu, pamoja na “maneno yake”.

Suala ni kwamba nasema hayo yote nikiendelea na tafakuri yangu, kama nikionacho sicho, je nikae kimya kwasababu kazi imeshaisha ilhali nikiona dhahiri shahiri imeisha ndivyo sivyo? Unajua kupitia runinga pale jukwani nilikuwa nawangalia baadhi ya waheshimiwa ambao walitoa maoni, nayakumbuka maoni yao, na baadaye walibadili msimamo na wakaunga mkono mambo tofauti na maoni yao. Nikajiuliza, waheshimiwa wale, furaha yao iko wapi, amani yao iko wapi, uaminifu wao uko wapi? Nikaendelea kujiuliza au ndio uongozi ulivyo? na kudhihirisha ule usemi usemao “kua uyaone”?

 Nakumbuka katika mojawapo ya vikao vya Tume ya Katiba vya mwishoni kabla ya Tume kuvunjwa, tulikuwa na mjadala mzito, wajumbe walikuwa wakitafakuri kwa pamoja mapokeo mabaya ya Rasimu Toleo la Pili hasa miongoni mwa watawala. Kwa uchungu nilisimama na kusema “kama tumesema uongo katika kazi ya Tume, basi tunapaswa kuhukumiwa daima, sasa na vizazi vijavyo, na kama tumefanya kazi ambayo wananchi wametutuma kwa mujibu wa sheria basi tunapaswa kuisimamia, na kusema ukweli daima”. Nitasema kweli daima juu ya ninachokijua kuhusiana na Mchakato wa kuandika Katiba Mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Nitakaa kimya nikisaidiwa majibu ambayo yamejengwa katika hoja na sababu, kwasababu huo ndio ulikuwa msingi wa mjadala wa kupata Katiba Mpya.

Tofauti ya Rasimu ya Warioba na Katiba Inayopendekezwa

Nijielekeze kwenye maeneo matatu ili kuonesha tofauti hizi kubwa:

(1)        Tunu za Taifa

Rasimu ya Mhe. Warioba ilipendekeza kuwa Jamhuri ya Muungano iwe na Tunu zifuatazo (a) utu; (b) uzalendo; (c) uadilifu; (d) umoja; (e) uwazi; (f) uwajibikaji; na (g) lugha ya Taifa, ambazo sisi sote kama Taifa tutazienzi na kuzizingatia. Tunu hizi au kwa kiingereza huitwa “national societal core values” ndio ambazo kila mtanzania angefanya awezavyo kuziishi ili kuwa na jamii ya kitanzania yenye maadili. Wamefuta yote na kubakisha utu na lugha ya Kiswahili. Najiuliza hivi kuna utu pasina uadilifu, uwajibukaji, umoja na uzalendo?

(2)        Maadili na Miiko ya Viongozi na Watumishi wa Umma

 Ibara Mahususi zifuatavyo zimetupiliwa mbali, Zawadi katika Utumishi wa Umma. Akaunti nje ya nchi na mikopo. Wajibu wa kutangaza mali na madeni. Mgongano wa maslahi na Matumizi ya mali ya umma kwa uchache katika eneo la Maadili na Miiko ya viongozi na watumishi kwa kigezo cha kutungiwa sheria ya Bunge.

 Kifungu cha Utii wa Miiko ya Uongozi wa Umma ambacho kilisema “21(1) bila ya kuathiri masharti ya Katiba hii, kiongozi wa Umma atapaswa kuheshimu na kutii maadili ya viongozi wa umma, ikiwemo Miiko ya Uongozi.

 (2) Miiko ya Uongozi inayorejewa katika ibara ndogo ya (1), itakuwa kama ifuatavyo: (a) Kiongozi wa umma hatopaswa - (i) kuvunja au kukiuka masharti ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano; (ii) kutoa au kupokea rushwa; (iii) kujilimbikizia mali kinyume cha sheria; (iv) kusema uongo au kutoa taarifa zisizo za ukweli; (v) kutoa siri za Serikali kinyume cha sheria; (vi) kutumia wadhifa, nafasi au cheo chake kwa manufaa yake binafsi, familia yake, ndugu, jamaa au marafiki            zake au mtu yeyote aliye na uhusiano naye wa karibu; (vii) kufanya vitendo vya uzembe, uvivu, ubaguzi, kiburi, dharau au unyanyasaji wa kijinsia.

 (b) Kiongozi wa umma atapaswa kuheshimu na kuendeleza - (i) dhana ya uwajibikaji wa pamoja kwa viongozi wanaohusika; na (ii) maadili na Miiko ya Uongozi wa Umma, ikijumuisha: (aa) kuwa na tabia na mienendo inayokubalika katika jamii; (bb) kuheshimu, kutunza na kulinda mali za umma; na (cc) kutambua, kuheshimu na kuzingatia Kanuni za Maadili na Mienendo ya Watumishi wa Umma, Kanuni za Kudumu za Watumishi wa Umma, nyaraka za umma na miongozo mbalimbali ya Serikali kuhusu viongozi na watumishi wa umma. (iii) kutenganisha biashara na shughuli binafsi na masuala yanayohusiana na uongozi.

 (3) Kiongozi wa umma ambaye anatuhumiwa kwa makosa ya: (a) kimaadili; (b) udhalilishaji wa mtu au wa kijinsia; au (c) wizi au ubadhirifu wa mali za umma, atasimamishwa kazi hadi suala lake litakapoamuliwa kwa mujibu wa sheria za nchi au taratibu nyingine zinazowahusu viongozi wa umma.” Ibara hii Mahususi imebaki kwenye historia kwamba imebaki katika Rasimu ya Warioba lakini Bunge Maalum katika kuiboresha imeifutilia mbali.

 (3)        Mapato ya Jamhuri ya Muungano

 Hili ni eneo ambalo litatuletea shida muda si mrefu kwa jinsi lilivyo katika Katiba Inayopendekezwa. Tunasema vyanzo vya Jamhuri ya Muungano ni Kodi ya Mapato, ushuru wa Bidhaa na Ushuru wa Forodha. Pendekezo hili limebaki kama lilivyo katika Katiba ya Mwaka 1977. Kimsingi na kwa ufupi, pendekezo hili halijawahi kutekelezeka tangu mwaka 1984, viongozi tujiulize kulirejesha kama lilivyo pasina ya kutoa hoja na sababu zinazokubalika katika pande zote za Jamhuri ni ubabe au ni kupanga kushindwa? Au kiingereza tunasema “planning to fail”. Nimejifunza kitu kuhusu watanzania waishio Zanzibar, wewe walazimishe na kwa shinikizo kubwa, watakukubalia katika misingi ya “funika kombe mwanaharamu apite” na kwa hakika wakirudi Zanzibar hawatatekeleza na itakuwa historia nyingine inayojirudia.

 Ninasema kwa ushahidi kwamba pendekezo hili litaendelea kuleta mzigo Tanzania Bara na litawaumiza wazanzibari. Nijielekeze kwenye mapato ya Zanzibar, kwa takwimu za makusanyo kutoka Zanzibar kupitia Bodi ya Mapato ya Zanzibar (ZRB) pamoja na Mamlaka ya Mapato ya Tanzania (TRA), kodi ya Mapato kwa Mwaka 2010/2011 kwa Zanzibar ni Bilioni 65.5 sawa na asilimia 36.1 ya Makusanyo yote ya Zanzibar ambayo yalikuwa Bilioni 180. Naomba mchumi daraja la kwanza anisaidie kuelewa, kama wazanzibari wamechukua mambo yao yote ya kiuchumi, je mambo hayo watayaendesha kwa mapato yepi kama zaidi ya asilimia 36 ya mapato yao yamechukuliwa na Jamhuri ya Muungano?

Makala hii ilitolewa na Humphrey Polepole katika Gazeti la Mwananchi la Jumapili Oktoba 12, 2014

Nimeanza kazi

Nimeanza kazi ya kuyaweka katika maandishi Mambo 100 ya wananchi yaliyotupwa na pamoja na makosa 50 ya kiuandishi ya Katiba Inayopendekezwa. Ombi si lazima likubaliwe, ila ombi langu ni kwenu ninyi kusoma na kufuatilia na kulinganisha wenyewe na mkiuona ukweli tunao usema basi msione haya kuisimamia kweli kwa faida ya Taifa letu leo na kwa ajili ya vizazi vijavyo
Karibuni pia kutizama video fupi ya mdahalo wa Katiba wa Mlimani City. Asante. Bado tunaweza kupata Katiba Bora, Ukimaliza sambazia na wengine wengi zaidi.




ASANTENI SANA NA MUNGU AWABARIKI ZAIDI NA ZAIDI

Naomba kuchukua fursa hii kuwashukuru wapendwa wote mlionitakia heri katika siku yangu ya kuzaliwa. Mungu awabariki zaidi na zaidi. Hata kama hatuonani kila siku lakini hilo halipotezi ukweli kwamba sisi ni marafiki wa kweli na tutabaki hivyo.
Tafakuri yangu katika siku ya kuzaliwa: Huyu anayeitwa Yesu Kristo, katika utumishi wake hapa duniani zaidi ya miaka 2000 iliyopita, alitumia miaka 3 kufanya yote aliyoyafanya na kutuachia legacy (urithi) ambao ni uhalisia na unaishi hata leo na utaendelea kubaki hivyo kwa vizazi vijavyo.
Baada ya pekua pekua, nilishafahamu na nikatumia muda kutafakari ufahamu huu, kwamba kwa yote aliyoyatenda Yesu Kristo akiwa hapa duniani aliyatenda akiwa kijana, tena kijana kwa mujibu wa Sera ya Vijana ya Mwaka 2007. Yesu Kristo alianza kufanya kazi yake akiwa na miaka 30 na aliitenda kwa miaka takribani 3 na kuhitimisha kazi yake akiwa na miaka 33.
Hoja yangu hapa si kujadili juu ya Yesu ni nani na utumishi wake duniani, hoja yangu ni tafakuri kwetu vijana, Je mpaka sasa tumejiwekea malengo ya kutimiza? Je tungesema tufunge hesabu zako leo unadhani ungekuwa umetusaidiaje wanadamu? Hivi ungekuwa umetuachia nini cha kukukumbuka? Tuache wanadamu wa dunia nzima, tuseme, basi watanzania, au watanzania ni wengi tuseme mtaani kwako, na mitaa nayo ni mikubwa, tuseme kazini, kijiweni, shuleni kwako, kwa rafiki, ndugu na jamaa zako.
Je tunaishi kwa malengo, je tunayaishi malengo yetu? Je tuna ndoto? Ulitaka kuwa rubani, je unaelekea huko? Ulitaka kuwa mwanamuziki, je unapiga hata ala mbili tatu kwa uhodari? Je unaelekea elekea huko? Ulitaka kuwa mtu mwenye mchango kwa shule, jamii au Taifa lako, mchango wa aina yoyote ile, Je umeanza kutoa mchango wako.
Simamia ndoto zako, ishi malengo yako na enenda katika namna ambayo itakufikisha katika tarajio lako tarajiwa kama mtu mwenye mchango kwa jamii yako. Kumbuka tunakua pamoja, Rai yangu kwetu sote, kwa uhalali na dhamira safi tujitahidi kuwezeshana ili tukue pamoja, tufanikiwe pamoja, asipatikane mmoja kuwa mzigo miongoni mwetu, kila mmoja wetu awe fursa, awe ngazi, awe kivuko, awe mlango, awe ufunguo wa mafanikio ya mwingine. Huo ndio utu wa kweli.
Ndoto zetu zitakuwa uhalisia tukiwa na Katiba Mpya na Bora ambayo inayokana na Maoni yetu na sisi tukiwa waandishi wakuu maana huo ndio mustakabali wetu. Isome Katiba Inayopendekezwa na uilinganishe na Rasimu ya Warioba, kisha ukishajiridhisha tujadiliane kwa hoja na sababu.
Mwisho ukimaliza kusoma tafakuri yangu ya Siku ya Kuzaliwa, Jiulize je Umeshajiandikisha kupiga kura kwa uchaguzi wa Serikali za Mitaa? Kama bado tafadhali nenda upesi, kama tayari pita tena ukathibitishe kama jina lako liko. Pia usisahau kufuatilia huyu "escrow" na uwe na uwezo wa kufuatilia hoja kadhaa kwa wakati mmoja bila ya kuondolewa kwenye reli ya hoja za msingi. Tanzania itajengwa na wenye Moyo na Imani.
Sambaza Uzalendo, huu ndio upendo kwa Taifa letu.